TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
FEBUARI 2, 2015
Tanzania kuwa Mwenyeji wa Sherehe za Utume
FEBUARI 2, 2015
Tanzania kuwa Mwenyeji wa Sherehe za Utume
Kanisa la Waadventista wa Sabato, Kanda ya Afrika Mashariki na Kati (ECD) limelipatia heshima Kanisa la Waadventista wa Sabato Tanzania kuwa mwenyeji wa Sherehe za Utume zitakazofanyika katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam, kuanzia Febuari 4 -7, 2015. Tanzania inapewa heshima hii kutokana na kudumisha sifa yake ya ukarimu pamoja na amani na utulivu.
Sherehe hizi, ambazo ni kubwa kuliko zote zilizowahi kufanyika katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati zinatarajiwa kuhudhuriwa na zaidi waumini 50,000 toka mataifa 11 yanayounda ukanda huu. Waumini hao wanatoka katika nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Eritrea, Somalia, Ethiopia, Sudan ya Kusini na Djibouti. Sherehe hizi pia zitahudhuriwa na zaidi ya viongozi 400 kutoka ukanda huu na viongozi toka makao makuu ya Kanisa la Waadventista wa Sabato duniani, wakiongozwa na Kiongozi wa kanisa hili duniani Mch. Ted Wilson. Sherehe kubwa za namna hii zilifanyika kwa mara ya mwisho Agosti 28 -31, 2013 katika kisiwa cha Jeju, huko Korea ya Kusini na baadaye zilifanyika Agosti 16, 2014 huko Manaus, nchini Brazil, katika bara la Amerika ya Kusini.
Katika sherehe hizi, zenye kauli mbiu ya “Kusherehekea Mibaraka ya Mungu katika Utume,” kanisa linajivunia mafanikio makubwa lililoyafikia katika upelekaji wa injili na utuoaji wa huduma kwa jamii.
Sherehe hizi zitapambwa kwa nyimbo zitakazoimbwa na zaidi ya kwaya 100, mahubiri, maombi kwa watu wenye shida mbalimbali, maombi ya kuliombea taifa, program za vijana, na program zingine mbalimbali. Pia kutakuwa na huduma za kijamii zitakazotolewa bure. Huduma hizo ni upimaji wa magonjwa ya moyo, sukari, ukimwi, na magonjwa mengine. Pia kutakuwa na upimaji wa damu pamoja na utoaji wa damu kuchangia benki ya damu ya Taifa.
Kupitia shirika lake la misaada, Adventist Development and Relief Agency (ADRA), kanisa litaunga mkono jitihada za serikali za uboreshaji wa maabara, kwa kutoa vifaa kwa ajili ya maaabara za Fizikia, Kemia, na Baolojia kwa moja ya shule za sekondari za jijini Dar es salaam.
Watu wote wanaalikwa kuja kuabudu na kufurahi katika sherehe hizi kubwa pamoja na kupata huduma bure za kijamii zitakazotolewa wakati wa mikutano hii.
Kanisa la Waadventista wa Sabato ni miongoni mwa makanisa ya Kiprotestanti, lenye makao makuu ya kiulimwengu huko Maryland, Washington, nchini Marekani. Hapa Tanzania Kanisa la Waadventista wa Sabato lina waumuni wapatao 5,000,000.